Kamati ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imemhoji mbunge wa Shinyanga Mjini (CCM), Stephen Masele kuhusu tuhuma zinazomkabili za utovu wa nidhamu.

Masele alihojiwa na kamati hiyo inayoongozwa na  Emmanuel Mwakasaka  jana Jumatatu Mei 20, 2019.

Mara baada ya kutoka katika mahojiano Masele alizungumza na wanahabari, “Mimi ninaheshimu  sana viongozi wangu, nimelelewa vizuri na wazazi, nimelelewa vizuri na chama changu, nimetokea umoja wa vijana kuanzia ngazi ya chini kabisa mpaka ngazi ya kitaifa na kuwa mjumbe wa baraza kuu Taifa, nimekuwa mbunge hii awamu ya pili.

“Nimekuwa naibu waziri  natambua miiko ya uongozi, sijawahi kukurupuka, fuatilia rekodi zangu chochote ninachokisema ninasimamia haki, ukweli na ninaheshimu viongozi wenzangu.

“Ni matarajio yangu haki itatendeka na mimi sijafanya jambo lolote kinyume na taratibu, kwenye kazi zangu ndani ya Bunge na pia Bunge la Afrika kama makamu wa rais.”

Kuhusu utovu wa nidhamu amesema, “Nawahakikishia Watanzania, nilichokuwa nasimamia ni misingi ya haki za binadamu na kufanya hivyo nisitafsiriwe kwamba ni utovu wa nidhamu.”