Vifo vitokanavyo na uzazi vimeongezeka Zanzibar, ikiwa ni nje ya mategemeo ya vifo vilivyotegemewa kutokea, kwa mujibu wa ripoti ya mwaka jana.

Kwa mujibu wa Abdulrahman Kwaza, Msaidizi wa  Mkuu wa Kitengo Cha Elimu ya Afya Zanzibar, wanawake 191 wanapoteza maisha kati ya vizazi hai 100,000, kinyume na matarajio ya vifo 110 kati ya vizazi hai 100,000 ambavyo zilitegemewa.

Hayo aliyasema wakati akiwasilisha mada katika semina ya ‘Jiongeze Tuwavushe Salama’ kwa viongozi wa dini wa Zanzibar.

Semina hii, ambayo imeratibiwa na kampuni ya True Vision Production (TVP) kwa kushirikiana na UNICEF Tanzania na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, ni sehemu ya mwendelezo wa semina nyingine tatu zilizofanyika Tanzania Bara hivi karibuni na kuhusisha pia viongozi wa dini tofauti, waandishi wa habari na wahariri.

Kwaza amesema vifo hivyo vinasababishwa na mambo mengi, ikiwemo umbali wa vituo vya afya, ukosefu wa wahudumu wenye utaalamu wa  kuzalisha na ukosefu wa elimu ya afya ya uzazi, vikichangiwa na membo mengine mengi.

Amesema ushiriki wa jamii katika afya ya uzazi umekuwa mdogo, huku akitoa wito wa kuimarisha huduma za kujifungua chini ya wataalamu wa afya, uboreshwaji wa vituo vya afya na kuweka msisitizo katika lishe ya mama akiwa mjamzito na ya mtoto baada ya kuzaliwa.

Amesema kitaalamu mama anatakiwa kumnyonyesha mtoto wake miezi 6 tangu anapozaliwa, kwani maziwa ya mama yanavirutubisho tosha vya kumlinda mtoto.

Amesema jitihada zimekuwa zikifanyika, huku akiongeza kuwa huduma za afya ya uzazi wa mpango zinapatikana katika vituo vingi, lakini bado kuna changamoto kwani baadhi ya vituo hivyo havitoi huduma za upasuaji mdogo.

Mtaalamu wa mawasiliano kutoka UNICEF, Usia Nkoma amesema jamii kwa ujumla ina wajibu wa kuhakikisha mama mjamzito anakwenda kliniki na kujifungua katika kituo cha afya na anatakiwa awe chini ya uangalizi wa wataalam wa afya masaa 48 baada ya kujifungua.

Sheikh Fadhil Soraga, ambaye ni katibu wa Mufti wa Zanzibar amesema viongozi wa dini wana dhamana ya kuhakikisha wanaelimisha jamii juu ya umuhimu wa kuokoa vifo vitokanavyo na uzazi.

Amesema Qur-an, kitabu cha Waislam, kina sisitiza juu ya afya ya uzazi, kikimtaka mama aliyejifungua kumnyonyesha mtoto wake miaka miwili iliyotimia ili awe na afya njema.
Naye Farashuu Khamis Musa kutoka ofisi ya Mufti amewashukuru waandaaji wa semina, akisema wataleta chachu ya kuokoa vifo hivyo.

“Viongozi wa dini wana wafuasi wengi, hivyo naamini watafanikiwa katika vita hii’, amesema Farashuu.
Mtaalamu wa Mawasiliano kutoka UNICEF Usia Nkoma akichangia mada katika semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama iliyofanyika Zanzibar
 Katibu wa Mufti - Zanzibar Sheikh Fadhil Soraga akizungumza katika semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama iliyofanyika Zanzibar
 Abdulrahman Kwaza,Msaidizi Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Afya Zanzibar akichangia mada katika semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama iliyofanyika Zanzibar
Farashuu Khamis Musa kutoka ofisi ya Mufti Zanzibar akichangia hoja katika semina ya Jiongeze Tuwavushe Salama iliyofanyika Zanzibar hivi karibuni