Dar es Salaam. Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Aga Khan, Eunice Pallangyo amefanya utafiti katika wilaya ya Ilala na kubaini kwamba vifo vya akinamama wilayani humo husababishwa na mambo mbalimbali, ikiwamo kutokuwepo huduma ya uangalizi baada ya kujifungua.

Akizungumzia utafiti huo leo Jumanne, Julai 11, Dk Pallangyo amesema amebaini hayo, baada ya kutembelea vituo vya afya na hospitali 27 za wilaya hiyo. Amesema huduma hiyo haitolewi ipasavyo licha ya mwongozo wa wizara ya afya kuagiza hivyo.

Dk Pallangyo amesema takwimu za wizara zinaonyesha kwamba wanawake 556 kati 1000 hufariki kwa sababu ya matatizo wakati wa kujifungua “Wanawake huondoka hospitali saa chache baada ya kujifungua bila kufanyiwa uchunguzi wa mara kwa mara,” amesema.

Amesema mwongozo wa wizara unataka mwanamke aliyejifungua kuchunguzwa mara kwa mara katika kipindi cha siku 42 za mwanzo. Amesema watoa huduma aliozungumza nao wamesema hawatoi huduma hiyo kwa sababu ya upungufu wa wafanyakazi na ufinyu wa nafasi katika vituo vya afya.

Hata wazazi waliohojiwa wengi walionyesha kutokuwa na elimu sahihi ya masuala ya uzazi.
"Kwa hiyo serikali imeweka miongozo ambayo watendaji wake hawaitekelezi kwa sababu ya changamoto zilizopo."Amesema.


Source: Mwananchi