Polisi watano wauawa Dallas, Marekani
Maafisa watano wa polisi mjini Dallas, Marekani wamepigwa risasi na kuuawa wakati wa maandamano ya kupinga mauaji ya watu weusi.
Maafisa wengine sita wanauguza majeraha.
Maafisa wa polisi katika mji ulio katika jimbo la Texas, wanasema mauaji hayo yametekelezwa na washambuliaji wawili wa kulenga shabaha.
Mkuu wa polisi wa Dallas David Brown amesema amesema maafisa wa polisi bado wanakabiliana na mshukiwa mmoja ambaye anadaiwa kujibanza katika jumba linalotumiwa kuegesha magari.

“Mshukiwa huyo ambaye tunawasiliana naye amewaambia maafisa wetu kwamba mwisho unakaribia na kwamba ataumiza na kuua wenzetu wengi, akimaanisha maafisa wa usalama na kwamba kuna mabomu yaliyotegwa eneo lote, kwenye gereji na katikati mwa jiji.”

Vyombo vya habari jimbo hilo vinasema kumetokea mlipuko mkubwa eneo hilo lakini habari hizo hazijathibitishwa.

Bw Brown amesema mwanamke aliyekuwa karibu na eneo alimojificha mwanamume huyo anahojiwa na maafisa wa usalama.





“Hatuwezi kusema kwamba tumewakamata washukiwa wote,” alisema mkuu huyo wa polisi.
Ufyatuaji risasi ulitokea mwendo wa saa tatu kasorobo usiku saa za Texas waandamanaji walipokuwa wakipitia barabara za mji na kuwafanya waandamanaji kukimbilia usalama wao.

Maandamano hayo yalitokana na kuuawa kwa wanaume wawili weusi, Philando Castile jimbo la Minnesota na Alton Sterling eneo la Baton Rouge jimbo la Louisiana.
Miongoni mwa maafisa wa polisi waliofariki ni afisa wa trafiki Brent Thompson, 43. 

Takwimu kutoka kwa shirika linalotetea maafisa wa polisi Marekani la Officer Down Memorial zinaonesha maafisa 53 wa polisi wameuawa wakiwa kazini mwaka 2016, 21 wakiuawa kwa kupigwa risasi. Idadi hiyo haijumuishi maafisa waliouawa Dallas.