Mwanamuziki 2 Face Ampa Shavu Vanessa Mdee 


2 Face Ampa Shavu Vanessa Mdee

MWANAMUZIKI mwenye jina kubwa Afrika, 2 Face Idebia amempa shavu la mwaliko diva anayekimbiza kwenye Tasnia ya Muziki Bongo, Vanessa Mdee ‘V Money’ kwenye tamasha lake litakalofanyika leo jijini Nairobi, Kenya huku wasanii mbalimbali kutoka kila kona ya Afrika wakitarajia kufanya makamuziki ya ukweli.

Akizungumza na moja ya gazeti maarufu nchini, V-Money anayetamba na Wimbo wa Niroge kwa sasa amesema shavu hilo kwake ni kitu kizuri maana kimeonesha ni jinsi gani wasanii wa nje wanavyothamini kazi zake hata kuamua kumpa mwaliko ambao mbali na kutangaza ngoma yake ya Niroge atapata fursa ya kukutana na wasanii wengi ambao anaweza kupata wa kufanya nao kazi.

“Namshukuru Mungu kazi zangu zinaheshimika, mwaliko wa 2 Face ni muhimu kwangu na nimeuchukulia kwa uzito kutokana na tamasha lenyewe litakavyokuwa kubwa, nina uhakika sitaondoka bure, lazima nitapata lolote la kufanya kwa mashabiki wangu,” alisema V- Money.