Kigwangalla Amtaka Gardner Aombe Radhi kwa Kumdhalilisha Lady Jaydee

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Hamis Kigwangalla, amemtaka mtangazaji wa Clouds FM, Gardner G Habash kumuomba radhi aliyekuwa mke wake, Lady Jaydee kwa ‘kile alichokiita’ kama udhalilishaji kwake na kwa wanawake wote.

Wikiendi iliyoisha imesambaa video mtandaoni ikimuonesha mtangazaji huyo akiongea kwenye tamasha alilokuwa mshereheshaji: "My name is Captain Gardner G Habash all the way from Clouds FM, Jahazi hatari sana. Na sina neno na yule mtoto wa kike. Nimeshamkojoza kwa miaka kama 15 hivi.”

Video hiyo imesababisha hasira kubwa kwa mashabiki wa Jaydee na watu wengi kwa ujumla.

“Ndg. Gardner amefanya udhalilishaji mkubwa si tu Kwa @JideJaydee bali ametukana wanawake wote. Mimi #BaloziWaWanawake namtaka aombe radhi,” ameandika mheshimiwa Kigwangalla kwenye Twitter.

“Natoa rai kwa uongozi wa @cloudsfm kumtaka Ndg. Gardner afute kauli yake na aombe radhi kwa @JideJaydee na kwa umma ili kulinda heshima yao,” ameongeza.

“Jamani, sijui ugomvi wao wala sina interest ya kujua, sema alichokisema G na nikasikia ni katika tusiyosemaga hadharani kwa heshima ya mama,” amefafanua.

“Sina maana wamchukulie hatua. Watambue tu kosa lake na wamtake kwa heshima kwa mama aombe radhi. Mimi ni mtumishi namba 2 kwenye Wizara inayosimamia ‘mambo ya wanawake’! I know what I am talking about hapa.”