Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Zelothe Steven amemwagiza Kamanda wa Polisi mkoa huo, Jacob Mwaruanda kuwasaka na kuwakamata watumishi hewa 18 waliobainika katika uhakiki uliofanyika katika halmashauri zote mkoani humo hivi karibuni.

Pia ameagiza fedha hizo zilizolipwa kwa watumishi hao hewa na kuiingizia hasara kubwa Serikali zirudishwe mara moja.

Akifafanua alisema katika uhakiki huo, watumishi hewa tisa walibainika katika wilaya ya Nkasi, wanane katika Manispaa ya Sumbawanga na mmoja wilaya ya Sumbawanga wakati Kalambo ikiwa haina mtumishi hewa.

Uhakiki huo unatokana na maagizo aliyotoa Rais John Magufuli baada ya kuwaapisha wakuu wa mikoa aliowateua, aliwaambia wakafanye kazi ya kutatua kero za wananchi na sio kwenda kufanya siasa.

Pia Rais Magufuli aliwapa wakurugenzi wa halmashauri siku 15 wawatoe katika orodha ya malipo ya mshahara wafanyakazi hewa wote katika halmashauri zote nchini.

Zelothe alitoa agizo hilo jana katika kikao maalumu cha kufahamiana kilichojumuisha wazee , viongozi wa dini , watendaji wa umma na wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa huo kilichofanyika mjini hapa.

Alisisitiza kuwa hajaridhishwa na uhakiki huo, hivyo akaagiza halmashuri zote kurudia upya uhakiki wa watumishi.

“Siku ile ile nilipoapishwa kabla sijavuka geti kutoka nje ya Ikulu nilipiga simu na kuagiza halmashauri zote (Manispaa, Nkasi, Kalambo na Sumbawanga) kuanza uhakiki mara moja wasinisubiri hadi niripoti mkoani hapa,” alieleza.

Aliongeza kuwa aliporudi mkoani humo na kuripoti kazini katika siku yake ya kwanza ofisini alikabidhiwa kitabu chenye orodha ya watumishi wa umma wa halmashauri zote akielezwa kuwa hakuna mtumishi hewa katika mkoa wa Rukwa.

“Sikukubaliana nao nilikataa, nikaagiza ufanyike uhakiki mara moja ndipo wamepatikana watumishi hewa 18 na watumishi wengine 137 wapowapo tu wakiwa na taarifa zinazotia mashaka. Wote wamebainika kwenye hicho kitabu nilichokabidhiwa kikionesha hakuna mtumishi hewa,” alisisitiza.